Topic: Makatazo Ya Kishari’ah Kwa Wanawake – 6 Katazo La Kujipiga piga Na Kuchana Nguo
Timeline: 2013-03-09 18:22:46
Imekusanywa Na: Abu Faatwimah
Makatazo Ya Kishari’ah Kwa Wanawake – 6 Katazo La Kujipiga piga Na Kuchana Nguo Wakati Wa Msiba
Katazo la Kuingia katika Hammamaat
[sehemu za kuogea zilizojengewa kama vile mahodhi mabwawa na kadhalika na kuruhusiwa kutumiwa na kila mtu].
Jamii nyingi huweka sehemu ambazo huwa zinaruhusiwa kutumiwa na kila mtu kwa malengo tofauti kama vile mabustani, maduni na kadhalika; pia hutenga sehemu nyingine ili zitumike kwa malengo maalumu; kama vile sehemu za kuogea au kuogolea, au sehemu za kuumika, au sehemu za kukandwa, au sehemu za kutengenezwa nyuso au nywele, au sehemu za kupambwa, au sehemu za kubadilisha mavazi au kujilinga, au sehemu za kupumzika, au sehemu za kufua nguo na kadhalika.
Sehemu hizi katika baadhi ya jamii huwa ziko zilizotengwa maalumu kwa wanawake na kutenganishwa na za wanaume, na katika jamii nyingine huwa hakuna mtengano katika sehemu kama hizo; hivyo utaona baadhi ya jamii hata katika hospitali zao huwa wanawaweka wagonjwa wa kike na wa kiume katika chumba kimoja na chenye kuwatenganisha huwa ni pazia tu, na wako wenye kudai kutaka kuweko choo cha wote [wake kwa waume] bila ya mtengano.
Dada yangu katika iymaan, ijapokuwa katazo hili linabeba jina la katazo la kuingia katika hammammaat [mahodhi], lakini linakusudia kueleza kukatazwa kwa Muumini wa kike kuingia katika sehemu yoyote ile ambayo atalazimika kujifunua mwili wake au kudhihirisha sehemu yoyote ile ya mwili wake isiyotarajiwa kudhihirika na kupelekea kuonekana na kila aliyepo katika sehemu hiyo ambae si maharimu wake au hata wanawake wenzake ambao si Waumini; au katika sehemu ambayo atalazimika kuvua au kujivua mavazi yake; iwe hijaab au nguo yake yoyote ile, au katika sehemu ambayo atalazimika kudhihirisha nywele zake. Sehemu zote zile anazokatazwa Muumini kuingia awe wa kike au kiume huenda zikawa za burudani -kama wanavyodai wengi- na nyingine, kama vile kwenye *****we [mwambao wa bahari], au sehemu za kuogelea (swimming pool), au saluni za kujiremba na kutengeneza nyuso au nywele; ni sehemu ambazo kwa kweli Muislamu wa kawaida huwa hatarajiwi kufikiria kwenda au kuweko kwa yale yanayofungamana na sehemu hizo, au kwa yale atayokutana nayo huko kwani hizo kwa ujumla ni sehemu zenye kila lenye kupingana na ile dini na shari’ah anayoshikamana nayo Muumini.
Hivyo, Muumini hatarajiwi kuwepo achilia mbali kuruhusu ahli zake na Waumini wenzake kuwepo, kama ilivyothibiti katika Hadiyth ya Jaabir (Radhiya Allaahu ‘anhu) kwamba Mjumbe wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:“Yeyote anayemuamini Allaah na Siku ya Mwisho asiingie kwenye hammaam isipokuwa [awe amevaa] nguo ya kiunoni, na yeyote yule anayemuamini Allaah na Siku ya Mwisho asimuingize –asimuachie kuingia- khaliylah [mke] wake hammaam, na yeyote yule mwenye kumwamini Allaah na Siku ya Mwisho asikae katika meza inayonywewa ulevi, na yeyote yule mwenye kumuamini Allaah na Siku ya Mwisho asikae faragha na mwanamke asiyekuwa mahramu wake, kwani watatu wao ni shaytwaan.”
[Imepokelewa na Ahmad, katika Musnad wake, katika Musnad ya Kumi waliobashiriwa Jannah, Saadis ‘ashar Al-Answaar, Hadiyth ya Jaabir bin ‘Abdillaah (Radhiya Allaahu ‘anhu), Hadiyth namba 14356].
Dada yangu katika iymaan, katika utumiaji wa mahodhi au mabwawa kama inavyoeleweka kuna uvuaji au ubadilishaji wa nguo au baadhi ya nguo na kudhihirisha mwili wote au sehemu ya mwili, ili mhusika aweze kuoga au kuogelea au japo kukaa ndani ya maji na kuburudika; ndio shari’ah ikamkataza Muumini kwenda kwenye hammamaat kama ilivyothibiti katika Hadiythi ya mama wa Waumini bibi ‘Aaishah (Radhiya Allaahu ‘anhaa) kwamba:“Mjumbe wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alikataza kuingia kwenye hammamaat, kisha akaruhusu Waumini wa kiume kuingia wakiwa wamevaa nguo za kiunoni”
[Imepokelewa na Abuu Daawuud, katika Kitabu cha Hammaam, Hadiyth namba 3497].
Na katika Hadiyth ya ‘Abdullaah bin ‘Amr (Radhiya Allaahu ‘anhu) Mjumbe wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:
“Hakika zitafunguliwa kwenu nchi za kigeni, na mtakuta humo nyumba kwa jina zinaitwa hammaamaat, basi wasiziingie wanaume isipokuwa kwa izaar –-wamevaa nguo ya kiunoni (vikoi): nguo yenye kufunika kutoka kitovu mpaka magoti- na akawazuia -kataza kuingia kwenye hammamaat- wanawake isipokuwa wanawake wagonjwa au wenye damu ya uzazi.”
[Imepokelewa na Abuu Daawuud, katika Kitabu cha Hammaam, Hadiyth namba 3499].
Hivyo asili ni kuwa mtu haruhusiwi kuingia kwenye hammaamaat au kwenda kwenye *****we na sehemu zenye kudaiwa kuwa ni za burudani kwani mwenye kuingia huko hulazimika kudhihirisha mwili au sehemu ya mwili wake kwa watu na kwa mwanamke huwa watu wasiokuwa maharimu zake, au hulazimika kuangalia watu wasio kuwa na nguo, na hili jambo limekatazwa kama ilivyothibiti katika Hadiyth ya Abu Sa’iyd Al-Khudriy (Radhiya Allaahu ‘anhu) amesema kwamba Mjumbe wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:“Mwanamme asitazame utupu wa mwanamme; na wala mwanamke asitazame utupu wa mwanamke; na wala mwanamme asilale na mwanamme mwenziwe katika nguo moja; na wala mwanamke asilale na mwanamke mwenzie katika nguo moja.”
[Imepokelewa na Muslim, katika Kitabu cha Hedhi, mlango wa uharamu wa kutazama sehemu za siri, Hadiyth namba 517].
Dada yangu katika iymaan, na hata kama itakuwa hiyo sehemu imetengwa kwa wanawake pekee, ieleweke kuwa huenda kukawepo wanawake wenzako ambao si Waumini kama wewe, na wasiokuwa Waumini huwa hawana cha kuwadhibiti, kwani asiyekuwa na iymaan au aliyekosa iymaan katika moyo wake na maisha yake hatarajiwi kuwa na kheri wala hayaa, na asiye na hayaa huwa hakuna cha kumdhibiti wala kudhibiti ulimi wake. Hivyo, dada yangu katika iymaan, katika hali kama hiyo kwenye hodhi au bwawa huwa umejifedhehesha na kujiondoshea mengi ya heshima na kubwa kuliko yote huwa umejiondoshea sitrah baina yako na Muumba wako, si tu kwa kuingia kwenye hodhi au bwawa, bali kwa kuvua nguo zako pahala ambapo si kwenye nyumba yako, jambo ambalo limekemewa na kukatazwa na shari’ah.Imethibiti katika Hadiythi kuwa baadhi ya wanawake kutoka Ash-Shaam waliingia kwa mama wa Waumini bibi ‘Aaishah (Radhiya Allaahu ‘anhaa); bibi ‘Aaishah (Radhiya Allaahu ‘anhaa) akawauliza: Mnatokea wapi nyiny?'
Wanawake wakajibu:
Sisi ni watu wa Ash-Shaam'. Bibi ‘Aaishah (Radhiya Allaahu ‘anhaa) akasema: Huenda nyinyi mnatoka katika kitongoji ambacho wanawake wake wanaingia katika hammamaat?' Wakasema: Ndio. Bibi ‘Aaishah (Radhiya Allaahu ‘anhaa) akasema: Hakika mimi nilimsikia Mjumbe wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akisema:”Mwanamke yeyote yule atakayevua nguo zake katika pasipokuwa nyumbani kwake -nje ya nyumba ya mumewe-, atakuwa amekwishachana kilichopo baina yake na baina ya Allaah.”
[Imepokelewa na Abuu Daawuud, katika Kitabu cha Hammaam, Hadiyth namba 3498; na At-Tirmidhiy, katika Kitabu cha Adab, mlango wa yaliyokuja katika kuingia Hammaam, Hadiyth namba 2747].
Dada yangu katika iymaan, na katika yenye kufanana na hammaam ambayo wanawake huwa wanapenda kutembelea na kwenda ni saluni za kujiremba na kutengenezwa nyuso, mwili na nywele. Sehemu hizi kama zilivyo ndugu yao hammaam huwa hazikosi kuwa na mambo mengi tu yenye kwenda kinyume au kupingana na shari’ah; kama vile unyoaji na unyofowaji wa nyusi, upigaji wa chapa, uunganishaji wa nywele, uvuaji na ubadilishaji wa nguo wenye kusababisha kutazama tupu, utoaji au unyofoaji na unyowaji wa nywele kwenye sehemu nyingine, ukataji au utengenezaji wa nywele wenye kufanana na mitindo ya kikafiri au mitindo ya wanawake wasiokuwa na heshima wala tabia nzuri, kutengenezwa au kupambwa na wanaume jambo ambalo ni msiba mkubwa na chanzo cha faahishah (uchafu).
Dada yangu katika iymaan, mtihani uliopo ni kuwa wanawake wengi wa zama hizi huwa wanafadhilisha na kupendelea kwenda kwenye sehemu hizi bila ya kuelewa kuwa ni sehemu zilizokatazwa kwa Muumin wa kike kwenda, huku wakielewa kuwa wasimamizi karibu wote au wengi wao ni watu wasiochunga heshima kwa Waumini hasa Waumini wa kike na wala hawako tayari kuwahifadhia siri zao, wachilia mbali kuwasitiri na kuwahifadhi tupu zao, na ukweli ni kuwa wengi wao ni katika mafasiki na wenye maradhi ya shahwaaniyyah na malengo yasiyo na heshima. Na wako katika wanawake wasiokuwa na hayaa wala heshima na wala hawajiheshimu nafsi zao, wenye kuwataka wanaume –wasiokuwa waume zao- kuwasugua, kuwakanda, kuwapamba, kuwatengeneza nywele, kuwapima na kuwalinga nguo na kadhalika; yote hayo ni katika vitangulizi vya faahishah.
Dada yangu katika iymaan, ni wajibu wako kuzihama sehemu hizi, sehemu zenye kuambatana na kupendwa na kila asiyekuwa na sehemu muhimu katika sehemu za iymaan ambayo ni hayaa, zihame sehemu zenye uvunjwaji wa heshima, sehemu zenye kusababisha mtu kukashifu tupu zake, sehemu zenye kumbaidisha mtu na kila lenye kupendwa na Allaah na Mjumbe Wake (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na kumkurubisha na kwenye kila lenye kuchukizwa na shari’ah; zihame na zihajiri mhamo na hijrah ya kishari’ah aliyokushauri Mjumbe wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kama ilivyothibiti katika Hadiyth ya ‘Abdullaah bin ‘Amru (Radhiya Allaahu ‘anhu) kuwa Mjumbe wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:
“Muislamu ni yule waliyesalimika Waislamu kutokana na ulimi wake na mkono wake; na Muhaajir ni yule aliyeyahama yale yaliyokatazwa na Allaah.”
[Imepokelewa na Al-Bukhaariy, katika Tafsiyr ya Qur-aan, Suurat Qul A’uwdhu bi Rabil Falq, Hadiyth namba 6032; na Ahmad, katika Musnad wake, katika Musnad ya Kumi waliobashiriwa Jannah, Musnad Al-Mukthiyriyna katika Swahaba (Radhiya Allaahu ‘anhum), Hadiyth ya ‘Abdullaah bin ‘Amru (Radhiya Allaahu ‘anhu), Hadiyth namba 6779].
Dada yangu katika iymaan, ni jukumu lako la kishari’ah kuwahadharisha wanawake wenzako katika iymaan, unaowaelewa miongoni mwa wale wenye tabia ya kutembelea sehemu hizo au kufikiria kuzitembelea, kwani hilo ni katika kuamrisha mema na kukataza munkari unalotarajiwa kujipamba nalo katika uhai wako; Allaah Anasema:“Na uweko (watokeze) kutoka kwenu Ummah unaolingania kheri na unaoamrisha ma’aruwf (mema) na unaokataza munkar. Na hao ndio waliofaulu.” [Aal-‘Imraan 3:104].
Katazo La Kujipiga piga Na Kuchana Nguo Wakati Wa Msiba Msiba ni katika Sunnah na mitihani ya uhai, Allaah Anasema: “Na bila shaka Tutakujaribuni kwa kitu katika khofu na njaa na upungufu wa mali na nafsi na mazao. Na wabashirie wenye kusubiri.” [Al-Baqarah 2: 155]. Pia Allaah Anasema:“Kila nafsi itaonja mauti. Na hakika mtalipwa kikamilifu ujira wenu Siku ya Qiyaamah. Basi atakayewekwa mbali na Moto na akaingizwa Jannah kwa yakini amefuzu. Na maisha ya dunia si lolote ila ni starehe ya udanganyifu.” [Aal-‘Imraan 3: 185].
Hii ni kusema kuwa hakuna njia ya kuuepuka kwa kuuchelewesha au kuukadimisha na wala hakuna njia ya kuukimbia; Allaah Anasema:“Popote mtakapokuwa yataku*****ieni mauti, japo mkiwa katika ngome madhubuti…” [An-Nisaa 4: 78]. Pia Allaah Anasema:“Sema: “Hakika [hayo] mauti ambayo mnayakimbia, bila ya shaka yatakukuteni…” [Al-Jumu’ah 62: 8] Dada yangu katika iymaan, msiba ni katika haki na ni miongoni mwa yale yaliyokwisha pitishwa na kukadiriwa na Muumba kuwa utamfikia mwanaadamu kama ulivyopanga na kwa wakati wake maalumu, Allaah Anasema: “Hautokei msiba katika ardhi na wala katika nafsi zenu isipokuwa umekwishaandikwa katika Kitabu kabla Hatujauumba…” [Al-Hadiyd 57: 22].
Hii ni kusema kuwa msiba hautokei kwa bahati mbaya, wala kwa makosa, na wala hauhitaji sababu, kwani hutokea kwa Elimu na Idhini yake Muumba; Allaah Anasema: “Na haiwi kwa nafsi yeyote kufa isipokuwa kwa Idhini ya Allaah, imeandikwa muda wake maalumu…” [Aal-‘Imraan 3: 145]. Dada yangu katika iymaan, kuyaelewa na kuyafahamu hayo na kuwa na iymaan thabiti kwayo si jambo jepesi wala si jambo rahisi na wala si jambo la kawaida, ndio Allaah Akaweka ujira mkubwa kabisa kwa kila mwenye kufikiwa na msiba kwa kuupokea kama Atakavyo Yeye kwa kutolalamika na kutonung’unika, bali kuridhika, kusubiri, kushukuru pale ataposema yale aliyoamrishwa na Allaah kama ilivyothibiti katika Hadiyth ya Ummu Salamah (Radhiya Allaahu ‘anhaa) kuwa Mjumbe wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:
“Hakuna Muislamu yeyote yule atakayekumbwa na msiba akasema yale Aliyomuamrisha Allaah: “Innaa liLLaahi wa innaa ilayhi raaji’uwn (hakika sisi ni wa Allaah na hakika sisi Kwake tutarejea).” [Al Baqarah 2: 156]. "Allaahumma Ajirniy fiy muswiybatiy Wakhluf-liy khayram-minhaa (Ee Allaah Nilipe –thawabu- kwa msiba wangu na nipe -badala yake- bora kuliko huo msiba)- isipokuwa Allaah Atampa badala yake bora kuliko huo msiba…” [Imepokelewa na Muslim, katika Kitabu cha Al-Janaaiz, mlango wa yenye kusemwa wakati wa msiba, Hadiyth namba 1531 na 1532].
Ujira na tunzo anayotunukiwa ni: “Hao juu yao zitakuwa Barakah kutoka kwa Mola wao na Rahmah, na hao ndio wenye kuongoka.” [Al-Baqarah 2: 157]. Tunzo hii imekusanya mambo matatu: Barakah kutoka kwa Mola, Rahmah na kuwa hao ndio Al-Muh-taduwn (walioongoka), kwa kusubiri kwao kwa msiba uliowashukia. Dada yangu katika iymaan, ni uzuri ulioje wa fadhila na malipo mema kutoka kwa Muumba Aliyechukuwa kile Alichomtunuku mja akasubiri na akashukuru na akaleta istirjaa’ -innaa liLLaahi wa innaa ilayhi raaji’uwn. Ama wenye kushindwa kusubiri, kushukuru na kuridhia majaaliwa na makadirio ya Allaah na wenye kudhani kuwa kilichochukuliwa ni chao, na kuwa hakikuchukuliwa bali wamepokonywa, huwa na mengi katika yenye kuonyesha na kuthibitisha kuwa si tu hawakuwa tayari, bali kubwa ni kuwa hawakufurahika kamwe, na wala hawakuridhika kamwe kwa msiba uliowasibu, bali huona na kuwa na hisia kuwa wameonewa, wamepokonywa na kunyang’anywa kilicho chao na kudhulimiwa.
Dada yangu katika iymaan, kutokana na mambo kama hayo na mingine mengi ya hayo ndio Waumini wakatakiwa wawe na subira wakati wowote ule wanaposibiwa na msiba si tu wa kuondokewa na vipenzi, kama ilivyothibiti katika Hadiyth ya Abu Hurayrah (Radhiya Allaahu ‘anhu) kwamba Mjumbe wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: “Amesema Allaah Aliyetukuka: Hana mja Wangu Muumini jazaa Nitakapomchukulia -Mfisha- mpenzi wake katika watu wa dunia, kisha akatarajia thawabu isipokuwa –atapata- Jannah.” [Imepokelewa na Al-Bukhaariy, katika Tafsiyr ya Qur-aan, Suurat Qul A’uwdhu bi Rabil Falq, Hadiyth namba 5973].
a pia katika Hadiyth ya Abu Muusa Al-Ash’ariyy (Radhiya Allaahu ‘anhu) amesema kwamba Mjumbe wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: “Anapofariki mtoto wa mja –katika Riwaayah ya Ibn Hibbaan: mja Muumin-, Allaah Husema: Ee Malaika wa mauti: Umechukua –katika Riwaayah ya Ibn Hibbaan na At-Tirmidhiyy: Allaah Huwaambia Malaika: Mmechukua- roho ya mwana wa mja Wangu? Umechukua kiburudisho jicho lake? Umechukua tunda la moyo wake! Malaika wa mauti husema: Na’am. Kisha Allaah Husema: Amesema nini mja Wangu? Malaika hujibu kuwa: Amekusifu –kwa kukuhimidi kwa kusema Al-Hamdu LiLLaahi-na amesema kauli ya istirjaa’ -innaa liLLaahi wa innaa ilayhi raaji’uwn-. Allaah Husema: Mjengeeni nyumba katika Jannah na iiteni Baytul-Hamd -nyumba ya shukurani-.” [Imepokelewa na Ahmad, katika Musnad wake, katika Musnad ya Kumi waliobashiriwa Jannah, tatimmat Musnad Al-Kuwfiyyiyna, Hadiyth ya Abu Muusa Al-Ash’ariyy (Radhiya Allaahu ‘anhu), Hadiyth namba 19286; na At-Tirmidhiyy, katika Kitabu cha Ijumaa, milango ya safari, Hadiyth namba 941, na amesema: Hii ni Hadiyth Hasanun Ghariybun; na Ibn Hibbaan, katika Kitabu cha Al-Janaaiz na yenye kufungamana nayo…, mlango yaliyokuja katika subira na thawabu za magonjwa, Hadiyth namba 3024].
Dada yangu katika iymaan, hayo ni baadhi ya malipo Aliyoyaandaa Mola ambayo hutarajiya kuwafikishwa kuweza kuyapata kila Muumin huko Aakhirah kwa kusubiri kwake; ama hapa duniani kuna ujira mkubwa pia na wenye kuvutia na kupendeza kwa kila Mudh-nibun na Mukh-twiun unapowafikia msiba wa kuondokewa na mpenzi au msiba wa aina nyingine yoyote ile kwa kusamehewa madhambi yao kwa kila kinachowasibu pindi wakisubiri na kutaraji malipo kama ilivyothibiti katika Hadiyth ya Abu Hurayrah (Radhiya Allaahu ‘anhu) kwambaMjumbe wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:“Muislamu hafikiwi na tabu wala machovu, wala hamu wala huzuni wala madhara, wala dhiki hata mwiba ukimchoma isipokuwa Allaah Humfutia kwayo makosa yake.” [Imepokelewa na Al-Bukhaariy, katika Kitabu cha Wagonjwa, mlango wa yaliyokuja katika kaffaar ya ugonjwa…, Hadiyth namba 5238 na 5239; na Muslim, katika Kitabu cha Al-Birr na Asw-Swilah naAadaab, mlango wa thawabu za Muumini katika yenye kumsibu miongoni mwa magonjwa…, Hadiyth namba 4674].
Dada yangu katika iymaan, ni uzuri ulioje wa fadhila na malipo mema ya Aakhirah na duniani kutoka kwa Muumba Aliyechukua kile Alichomtunuku mja, Mola Aliyeandika mja kufikiwa na tabu, machovu, hamu, huzuni, madhara, dhiki, maradhi, kuchomwa na mwiba na kadhalika, akasubiri, akashukuru na akasema yale aliyomuamrisha Mola wake. Dada yangu katika iymaan, kinachotakiwa kwa aliyefikwa na msiba ni kusubiri na kwa kila mwenye kwenda kutoa mkono wa pole –ta’ziyah- kusisitiza subira na kuhimiza kuridhika kwa yale Aliyoyapitisha Allaah na kumbashiria malipo makubwa yasiyokuwa na hesabu ya wanaosubiri; Allaah Anasema: “Hakika wanaosubiri watalipwa kikamilifu ujira wao bila ya hesabu.” [Az-Zumar 39: 10].
Dada yangu katika iymaan, ukweli ni kuwa si kila mwenye kufikwa na msiba huweza kufikia kuingia katika wale wenye kutarajia malipo makubwa na yasiyo na hesabu yaliyoahidiwa na Mola; dada yangu katika iymaan, mimi na wewe tunao mfano mzuri kwa mwanamke katika wenye subira yenye kupelekea kuweza kufikia daraja ya kutodhihirisha hata huzuni wakati wa msiba kama ilivyothibiti kwa Swahaabiyyah (Radhiya Allaahu ‘anhaa) miongoni mwa Swahaabiyyaat (Radhiya Allaahu ‘anhunna) wa Mjumbe wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kama inavyosimuliwa kuwa Anas bin Maalik (Radhiya Allaahu ‘anhu) alisikiwa akisema kuwa:“Abu Twalhah alifiwa na mtoto aliyezaa na Ummu Sulaym.
Ummu Sulaym akawaambia jamaa zake: “Msimweleze Abu Twalhah mpaka mimi niwe ndiye nitakayemweleza” Aliporudi, akampelekea chakula cha jioni, akala na akanywa, kisha –Ummu Sulaym- akajipamba kuliko anavyojipamba siku zote. Abu Twalhah akamjamii. Ummu Sulaym alipoona kuwa Abu Twalhah ameshiba na amemjamii alimwambia: “Ee Abu Twalhah! Niambie lau watu wameazima kitu kwa watu fulani, kisha walioazimwa wakataka kitu chao kilichoazimwa, je, walioazima wana haki ya kuwanyima?” Abu Twalhah akajibu: “Hapana!” Ummu Sulaym akamwambia: “Basi taraji thawabu kwa msiba wa mwanao.” Abu Twalhah akakasirika na akasema: “Umeniacha mpaka nimejichafua [kwa jimai] halafu ndio unaniambia habari ya msiba wa mwanangu?” Abu Twalhah akaenda kwa Mjumbe wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akamueleza mambo yalivyokuwa. Mjumbe wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akawaombea kwa kusema: “Allaah Awabarikie katika usiku wenu.” Ummu Sulaym akabeba mimba. Akazaa mvulana. Abu Twalhah akaniambia: “Mbebe umpeleke kwa Mjumbe wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam).” Akapeleka na tende kadhaa. Mjumbe wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akauliza: Ana kitu? Akajibu: “Ndio, tende kadhaa.”
Mjumbe wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akazichukua akazitafuna kisha akachukua zile tende zilokuwa mdomoni mwake akazitia katika kinywa cha mtoto, halafu akamsugulia nazo (ili mtoto afyonze na kumeza) na akampa jina la ‘Abdullaah…” [Imepokelewa na Al-Bukhaariy, katika Kitabu cha Al-Janaaiz, mlango wa asiyedhihirisha huzuni zake kwenye msiba, Hadiyth namba 1225; na Muslim, katika Kitabu cha fadhila za Swahaabah (Radhiya Allaahu ‘anhum), mlango wa katika fadhila za Abi Twalhah al Answaariy, Hadiyth namba 4503].
Dada yangu katika iymaan, huo ni mfano mzuri na wa aina yake wa kutodhihirisha huzuni wakati wa msiba wa kipenzi wenye kutaka kuigwa, na kuacha kuiga mifano ya wenye kushindwa kuvuta subira na kujizuia, jambo linalowapeleka kuanza kuwa kama waliopoteza fahamu na kurukwa na akili zao; hivyo utawaona wanajipiga piga, na wakati mwingine wanachana chana nguo zao na kubwa kuliko hayo yote ni huku kufunua midomo yao na kuanza kutoa matamshi ya kijaahiliyyah matamshi yasiyoridhiwa na kila mwenye chembe ya iymaan, wachila mbali Muumba.
Dada yangu katika iymaan, kuomboleza kijahili iwe kwa kujipiga piga mashavu au sehemu yoyote ile katika mwili, kujinyoa nywele au kuzivuta, kuchana nguo, kukwaruza uso na kujiapiza au kutamka matamshi ya kijaahiliyyah na maajabu ya dunia ikiwemo kujiombea mauti ni moja kati ya desturi na kawaida za kijahiliyyah ambazo bado zina nafasi kubwa katika baadhi ya nafsi za wengi miongoni mwa wenye kujiita Waislamu hasa wa kike wakisahau kuwa Mjumbe wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) ametuhadharisha na kutuwekea wazi uwazi wa mwangaza wa mchana kuwa ulimi –kupayuka kwetu- ndio unaopelekea kuadhibiwa au kurehemewa, hivyo tuchague lenye kheri nasi na kwa maiti wetu; Mjumbe wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: “Hakika Allaah Haadhibu kwa chozi la jicho, na wala kwa huzuni za moyo, lakini Huadhibu kwa huu akiashiri ulimi wake au Hurehemu…” [Imepokelewa na Al-Bukhaariy; katika Kitabu cha Al-Janaaiz, mlango wa kauli kwenye mgonjwa, Hadiyth namba 1228].
Dada yangu katika iymaan, katika kujaribu kuiondosha na kuing’oa desturi hii ya kijaahiliyyah Mjumbe wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) ameikemea kwa makemeo ya hali ya juu kwa kuwa huko ni kutokuridhika na kutoamini Qudra ya Muumba [nako ni kufru] na kutokuamini yaliyothibiti kwa kila aliyefikiwa na msiba akasubiri; hivyo desturi hii ya kijahili imekemewa makemeo yaliyo makali yenye kupelekea kuhakikisha kuwa kila Muislamu aliyefikiwa na msiba ajilazimishe kusubiri, subira itayompelekea kuweza kufikia kujichotea Aliyoyaandaa Allaah kwa wenye kusubiri na kuridhika na msiba uliomshukia, Mjumbe wa Allaah amefikia kusema kuwa ‘si katika sisi, kwa maana kuwa si katika Waumini’ kama ilivyothibiti katika Hadiyth ya Ibn Mas’uwd (Radhiya Allaahu ‘anhu) kuwa Mjumbe wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: “Si katika sisi mwenye kulia kwa kujipiga piga, kujichania nguo na kuomboleza kwa maombolezo ya kijaahiliyah.” [Imepokelewa na Al-Bukhaariy, katika Kitabu cha Al-Janaaiz, mlango wa si katika sisi mwenye kulia kwa kujipiga piga…, Hadiyth namba 1221 na 1222; na katika Kitabu cha Al-Manaaqib, mlango yenye kukatazwa miongoni mwa maombolezo ya kijaahiliyyah, Hadiyth namba 3281; na Muslim, katika Kitabu cha Iymaan, mlango wa Uharamu wa kujipiga piga na kujichana chana nguo, Hadiyth namba 151].
Dada yangu katika iymaan, la maajabu ni kuwa mtu kuingia katika Uislamu hutarajiwa kuwa amejivua na kujing’oa na yote aliyokuwa nayo ya kijaahiliyyah vinginevyo huwa bado hakuingia katika Uislamu kikamilifu kama Alivyoamrishwa na Muumba; Allaah Anasema: “Enyi mlioamini! Ingieni katika Uislamu kikamilifu, na wala msifuate hatua za shaytwaan. Hakika yeye kwenu ni adui wa wazi.” [Al-Baqarah 2: 208].
Dada yangu katika iymaan, Mjumbe wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu ‘anhum) na ni matarajio kuwa kila mwenye kuwafuata kwa ihsaan kuwa mbali umbali wa mbingu na ardhi na hizi mila za kijaahiliyyah kama ilivyothibiti katika kauli ya mmoja wa Swahaba zake (Radhiya Allaahu ‘anhu) kuwa: “Abu Muusa (Radhiya Allaah ‘anhu) alipokuwa mgonjwa taabani ghafla alizimia, na kichwa chake kikiwa katika chumba cha mwanamke katika ahli zake, basi mwanamke katika ahli zake akapiga kelele –kulia kwa sauti-, [Abu Muusa (Radhiya Allaah ‘anhu)] hakuweza kumrudi kwa chochote kile, alipozinduka, [Abuu Muusa] akasema: Mimi niko mbali –naepukana- na yale -matendo- yote aliyojiweka nayo mbali –aliyokataza na kuyakemea- Mjumbe wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam); kwani Mjumbe wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amejiweka mbali na Asw-Swaaliqah –mwanamke mwenye kulia kwa kunyanyua sauti yake na kupayuka kwa sababu ya msiba uliomshukia-, na [pia amejiweka mbali na] Al-Haaliqah –mwanamke mwenye kunyoa nywele zake kwa sababu ya msiba-, na [pia amejiweka mbali na] Ash-Shaaqah –mwanamke mwenye kupasua nguo zake sababu ya msiba-.” [Imepokelewa na Muslim, katika Kitabu cha Iymaan, mlango wa uharamu wa kupiga piga mashavu na kuchana chana nguo, Hadiyth namba 152 na 153]. Hadiyth iko wazi kabisa katika kukataza na kukemea:
1. Kulia kwa kunyanyua sauti na kupayuka
2. Kujinyoa nywele
3. Kuchana chana nguo na kujipiga piga wakati wa msiba.
Dada yangu katika iymaan, desturi hizi - mambo matatu haya- ni katika zenye kuonekana na kudhihiri kuwa ni zenye kupendwa na ni yenye nguvu na kuwa na washabiki wengi mpaka yakaonekana kuwa ni katika mafundisho ya Uislamu kwani ni katika mambo ya kawaida na ni yenye kukubalika kuwepo katika misiba kwa kuwa yanaonekana katika karibu misiba yote; yawe ya wenye kujiita Waislamu na Waislamu wa kawaida na hata wale wenye kudhaniwa kuwa ni wenye elimu au wenye kufikiriwa kuwa wanafuata mafundisho ya Mjumbe wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam).
Dada yangu katika iymaan, na kila Muislamu mwenye kumpenda Mjumbe wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake kiramu (Radhiya Allaahu ‘anhum) na kuwafuata kwa ihsaan; ukiwafikishwa kuusoma na kuuelewa waraka huu, ni vyema ushikamane na ujilazimishe kushikamana na mafundisho sahihi ya Mjumbe wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) katika maisha yako kwa ujumla na katika kila lenye kukusibu lenye kukupelekea kuhuzunika kwa kutoweka kwake au kulikosa; kwani ushauri wa Mjumbe wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) ni kuwa tushikamane na Sunnah zake na Sunnah za Makhalifa wake waongofu kama ilivyothibiti katika Hadiyth kuwa Mjumbe wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:“Nakuusieni kuwa na taqwah ya Allaah, na kusikiliza na kutii hata ikiwa –huyo kiongozi wenu atakayekuamrisheni- ni mtumwa wa kihabashi; kwani hakika atakaeishi miongoni mwenu baada yangu ataona –atakutana atapambana na – ikhtilafu nyingi; kwa hiyo shikamaneni na Sunnah zangu na Sunnah za Makhalifa Ar-Raashidiyn Al-Mahdiyyiyn -walioongoka-, shikamaneni nazo na ziumeni kwa magego -zikamateni kwa nguvu zenu zote wala msiziache-; na tahadharini na mambo ya uzushi, kwani hakika kila uzushi ni bid'ah –uzushi katika dini-, na kila bid’ah ni upotofu.” [Imepokelewa na Ahmad, katika Musnad wake, katika Musnad ya Kumi waliobashiriwa Jannah, Musnad Ash-Shamiyyiyna, Hadiyth ya Al-‘Ir-baadh bin Saariyah, Hadiyth namba 16815; na Abu Daawuud, katika Kitabu cha Sunnah, mlango katika kulazimu Sunnah, Hadiyth namba 3994; na At-Tirmidhiyy, katika Kitabu cha Elimu, mlango wa yaliyokuja katika kushikamana na Sunnah na kujiepusha na bida’h, Hadiyth namba 2620].
Dada yangu katika iymaan, tusizue wala tusiige na wala tusiipambe misiba yetu mambo ya kijaahiliyyah ambayo yaliyochopekwa na kupachikwa katika mafundisho ya Mjumbe wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na kupambiwa Waislamu kwa lengo la kuwapoteza na kuwabaidisha na mafunzo sahihi ya Mjumbe wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam); hivyo katika uhai wako wote yasikughururi yale yote yenye kufanywa na watu wasiokuwa Waislamu, na pia yale yenye kutendwa na kupigiwa debe na wale wanaojiita Waislamu ambao wako mbali na Sunnah za Mjumbe wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na mafundisho yake sahihi katika kawaida, na katika maisha yao hufanya kila jambo lililokatazwa na shari’ah bali huzua na kumzulia Mjumbe wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) wachilia mbali unapowasibu msiba wakati ambao hutumbukia na kung’ang’ania kila lenye kuzushwa bila ya kuelewa au kujali kuwa Mjumbe wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) ametutahadharisha kwa kusema:“Atakayetenda kitendo kisichokuwa na mafunzo ya dini yetu, hicho kitarudishwa.” [Imepokelewa na Al-Bukhaariy, katika Kitabu cha Al-Hajj, milango ya al Muhswir na jazaa ya kuwinda, Hadiyth namba 2513; na Muslim, katika Kitabu cha Al-Ak-dhiyyah, mlango wa kuvunja hukumu batili na kurudisha yenye kuzushwa., Hadiyth namba 3248 na 3249].
**{Legacy activities, comments etc counter: 4448; topic series: 6; forum: MediaSwahili; associated: 6- /*}